Utoaji Mimba Usio Salama Ni Jambo La Kawaida Nchini Tanzania Na Ni Sababu Kubwa ya Vifo Vya Wajawazito

Utafiti mpya Watoa Makadirio ya Kwanza Kitaifa ya Matukio ya Utoaji Mimba Nchini

Katika utafiti wakilishi wa kwanza kitaifa kuhusu matukio ya utoaji mimba na huduma baada ya kuharibika kwa mimba nchini Tanzania, watafiti waligundua kwamba utoaji mimba kwa siri hutokea mara nyingi na huchangia kwa kiasi kikubwa kwenye vifo na kuumia kwa wajawazito. Utafiti huo, uliofanywa na watafiti kutoka taasisi ya Guttmacher iliyoko Marekani, Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili zilizoko hapa Tanzania, waligundua ya kwamba makadirio ya mimba 405,000 zilitolewa nchini ndani ya mwaka 2013, nyingi zikitolewa kwa taratibu ambazo si salama na kuhatarisha maisha ya wanawake. Kutokana na mchanganyiko wa sheria tata na yenye vizuizi vingi ya utoaji mimba ya Tanzania, wanawake hutafuta huduma za utoaji mimba zinazofanyika kisiri na ambazo si salama.

Watafiti hao, ambao walifanya utafiti kwenye vituo vya afya, miongoni mwa wataalamu wa afya na kufanya mapitio ya taarifa za idadi ya watu na uzazi, wamekadiria kwamba wanawake 66,600 walipewa huduma baada ya kuharibika kwa mimba kwenye vituo vya afya kutokana na matatizo yaliyotokana na utoaji mimba usio salama ndani ya mwaka 2013. Hata hivyo, karibu wanawake 100,000 ambao walipata matatizo hawakupata matibabu ambayo waliyahitaji. Watafiti wanatumaini kwamba matokeo yao yatasaidia kutaarifu  juhudi zinazoendelea nchini Tanzania kupunguza uwiano wa vifo vya wajawazito, ambao umebaki kuwa miongoni mwa iliyo juu zaidi duniani.

"Kwa kutambua kuwa utoaji mimba usiokuwa salama ni chanzo kikuu cha vifo vya wajawazito, Serikali ya Tanzania imepanua wigo wa upatikanaji wa huduma baada ya kuharibika kwa mimba katika muongo mmoja uliopita, lakini mapungufu makubwa bado yapo na wanawake wengi hawapati huduma wanazohitaji," alisema Sarah C. Keogh, mtafiti mwanasayansi mwandamizi wa taasisi ya Guttmacher na mwandishi kiongozi wa utafiti huo. "Utafiti huu unabainisha mapungufu hayo na kusaidia kuunda mikakati kuhakikisha kuwa kila mwanamke wa Kitanzania anayehitaji anaweza kupata huduma baada ya kuharibika kwa mimba inayoweza kuokoa uhai."

Kiwango cha kitaifa cha utoaji mimba nchini Tanzania—36 kwa kila wanawake 1,000 walio kwenye umri wa uzazi—kinafanana na viwango vya nchi nyingine za Afrika Mashariki. Hata hivyo, ndani ya Tanzania viwango vya utoaji mimba vinatofautiana kwa ukanda. Viwango vya juu ya utoaji mimba hupatikana katika Kanda ya Ziwa (51 kwa kila wanawake 1,000) na Nyanda za Juu Kusini (47 kwa kila wanawake 1,000), na kiwango cha chini hupatikana Zanzibar (11 kwa kila wanawake 1,000). Viwango hivi tofauti vya utoaji mimba huhusishwa kimsingi na utofauti katika viwango vya matumizi ya njia za uzazi wa mpango na mimba zisizotarajiwa, na uwezekano wa wanawake kuamua kutoa mimba katika tukio la kupata mimba zisizotarajiwa.

"Mbali na huduma baada ya kuharibika kwa mimba, wanawake wa Kitanzania wanahitaji upatikanaji bora na kamilifu wa huduma mbalimbali za njia za uzazi wa mpango na ushauri nasaha kuhusu uzazi wa mpango  ili waweze kufanya maamuzi sahihi," alisema Godfather Kimaro, mwanasayansi mtafiti wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu nchini Tanzania, ambaye alifanya kazi kwenye utafiti. "Ndani ya mwaka 2013, wanawake wa Kitanzania walipata mimba zisizotarajiwa zaidi ya milioni moja, ambazo kati yake 39% ziliishia kwenye kutolewa. Kukabiliana na mahitaji yasiyokidhiwa ya uzazi wa mpango kutapunguza kiwango cha mimba zisizotarajiwa na hivyo kupunguza uhitaji wa kutoa mimba na vifo na majeruhi ambayo kwa mara nyingi hutokea baada ya taratibu zisizo salama."

Watafiti wamependekeza kuimarisha juhudi za kuhakikisha upatikanaji wa huduma baada ya kuharibika kwa mimba, ambayo kwa sasa inapatikana bila ulinganifu katika maeneo mbalimbali. Wamependekeza uwekezaji katika kufanya huduma baada ya kuharibika kwa mimba inapatikana katika ngazi zote za mfumo wa afya, ikiwa ni pamoja na kuwapa mafunzo watoa huduma wa ngazi ya kati na kusambaza kikamilifu dawa na vifaa vyote muhimu kwenye vituo vya afya. Pia, walisisitiza umuhimu wa kujumuisha utoaji wa huduma za uzazi wa mpango  kama sehemu ya huduma baada ya kuharibika kwa mimba na kuhimiza kwamba kila mwanamke anayetibiwa kutokana na matatizo yanayohusiana na kutoka kwa mimba apewe ushauri wa kina na nyenzo za uzazi wa mpango. Hatimaye, walipendekeza kwamba utata katika sheria ya utoaji mimba ya Tanzania ufafanuliwe kuhakikisha kuwa wanawake wanaweza kupata utaratibu salama na wa kisheria  kwa kiasi kamili kinachoruhusiwa. Watafiti wanatumaini kwamba matokeo ya utafiti huu yatasaidia kuleta mwanga kwenye sera na mipango ambayo italeta huduma za kifanisi zaidi na hatimaye kuboresha hali ya afya ya uzazi ya wanawake wote wa Tanzania.

"Matukio ya Utoaji Mimba na Huduma Baada ya Kuharibika kwa Mimba Nchini Tanzania" na Sarah C. Keogh wa Taasisi ya Guttmacher et al. inapatikana mtandaoni kupitia PLoSONE.

Utafiti huu uliweza kufanyika kutokana na misaada kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya Uholanzi, Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Serikali ya Uingereza, na Shirika la Ushirikiano wa Maendeleo la Norway.